Matendo ya Mitume 3:1-16 (OTB)
1Petro na Yohana walikuwa wakipanda kwenda hekaluni saa ya kusali, ambayo ilikuwa saa tisa. 2Mtu mmoja ambaye alikuwa kiwete tangu kuzaliwa alikuwa akibebwa hadi kwenye lango la hekalu liitwalo Mzuri, ambako aliwekwa kila siku kuomba sadaka kwa wale waliokuwa wakiingia katika viwanja vya hekalu. 3Alipowaona Petro na Yohana wakiingia katika viwanja vya hekalu, aliwaomba sadaka. 4Petro, pamoja na Yohana, walimtazama kwa makini na kusema, “Tutazame sisi.” 5Yule mtu aliwapa makini yake, akitarajia kupokea kitu kutoka kwao. 6Petro akasema, “Fedha na dhahabu sina, lakini kile nilicho nacho nakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama utembee.” 7Akamshika kwa mkono wa kuume, akamsaidia kusimama, na mara miguu yake na vifundo vya miguu vikapata nguvu. 8Akaruka kwa miguu yake na kuanza kutembea, akaenda nao katika viwanja vya hekalu, akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu. 9Kila mtu alimwona akitembea na kumsifu Mungu; 10na wakamtambua kuwa ndiye yule mtu aliyekuwa akiketi akiomba sadaka kwenye lango la hekalu liitwalo Mzuri, nao wakajawa na mshangao na kustaajabu kwa yaliyomtokea. 11Alipokuwa akiwashikilia Petro na Yohana, watu wote walikimbia pamoja kwao mahali paitwapo Nguzo za Sulemani, wakiwa wamepigwa na bumbuazi. 12Petro alipoona hili, akawahutubia watu, “Enyi watu wa Israeli, kwa nini mnashangaa kwa hili? Kwa nini mnatutazama kama kwamba kwa nguvu zetu wenyewe au utakatifu wetu tumemfanya huyu kutembea? 13Mungu wa Abrahamu, Isaka, na Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye mlimkabidhi na kumkana mbele ya Pilato, ingawa alikuwa ameamua kumwachilia. 14Mlimkana Yule Mtakatifu na Mwenye Haki na mkamwomba mwuaji aachiliwe kwenu. 15Mlimwua Mkuu wa uzima, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, na sisi ni mashahidi wa jambo hili. 16Kwa imani katika jina la Yesu, huyu mtu mnayemwona na kumjua ameimarishwa. Ni jina la Yesu na imani inayotoka kwake iliyompa afya kamilifu mbele yenu nyote.
Fungua katika kisoma Biblia ↗