Nehemia 8:1-12 (OTB)
1Watu wote walikusanyika pamoja kama mtu mmoja katika uwanja mbele ya Lango la Maji, nao wakamwomba Ezra mwandishi alete Kitabu cha Torati ya Musa, ambacho Bwana alikuwa amewapa Israeli. 2Basi Ezra kuhani akaleta Torati mbele ya kusanyiko, ambalo lilijumuisha wanaume, wanawake, na wote walioweza kuelewa, siku ya kwanza ya mwezi wa saba. 3Akasoma kutoka humo kwa sauti kuanzia asubuhi na mapema hadi adhuhuri mbele ya uwanja mbele ya Lango la Maji, mbele ya wanaume, wanawake, na wale walioweza kuelewa, na watu wote wakasikiliza kwa makini Kitabu cha Torati. 4Ezra mwandishi alisimama juu ya jukwaa la juu la mbao lililojengwa kwa ajili ya tukio hilo. Karibu naye upande wa kulia walikuwa Mattithia, Shema, Anaia, Uria, Hilkia, na Maaseia; na upande wake wa kushoto walikuwa Pedaia, Mishaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadana, Zekaria, na Meshulamu. 5Ezra akakifungua kitabu mbele ya watu wote, kwa kuwa alikuwa juu yao; na alipokifungua, watu wote walisimama. 6Ezra akamsifu Bwana, Mungu mkuu, na watu wote wakajibu, “Amina, Amina!” huku wakinyanyua mikono yao. Kisha wakainama na kumwabudu Bwana kwa nyuso zao chini. 7Walawi—Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodaya, Maaseia, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani, na Pelaia—walieleza Torati kwa watu wakati walipokuwa wamesimama mahali pao. 8Wakasoma kutoka katika Kitabu cha Torati ya Mungu, wakikifanya kiwe wazi na kutoa maana ili watu waelewe kilichosomwa. 9Kisha Nehemia liwali, Ezra kuhani na mwandishi, na Walawi waliokuwa wakiwafundisha watu wakawaambia wote, “Siku hii ni takatifu kwa Bwana Mungu wenu. Msiomboleze wala kulia.” Kwa maana watu wote walikuwa wakilia waliposikia maneno ya Torati. 10Nehemia akasema, “Nendeni, kuleni vyakula vizuri na kunyweni vinywaji vitamu, na mpelekeeni sehemu wale ambao hawakujiandalia chochote. Siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu. Msiwe na huzuni, kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.” 11Walawi wakawatuliza watu wote, wakisema, “Tulieni, kwa maana hii ni siku takatifu. Msiwe na huzuni.” 12Kisha watu wote wakaenda kula na kunywa, kugawana sehemu za chakula, na kusherehekea kwa furaha kuu, kwa sababu sasa walielewa maneno yaliyokuwa yameelezwa kwao.
Fungua katika kisoma Biblia ↗