1 Samweli 16:1-13 (OTB)
1Bwana akamwambia Samweli, “Je, utaomboleza juu ya Sauli mpaka lini, kwa kuwa nimemkataa asiwe mfalme juu ya Israeli? Jaza pembe yako kwa mafuta uende; ninakutuma kwa Yese Mbethlehemu, kwa maana nimemchagua mfalme kwa ajili Yangu kutoka kwa wanawe.” 2Lakini Samweli akasema, “Nitawezaje kwenda? Sauli akipata habari, atanipiga.” Bwana akasema, “Chukua ndama wa kike pamoja nawe na useme, ‘Nimekuja kutoa dhabihu kwa Bwana.’ 3Kisha mwalike Yese kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha cha kufanya; nawe utampaka mafuta Yule nitakayekuonyesha.” 4Basi Samweli akafanya kama Bwana alivyosema na kwenda Bethlehemu. Wazee wa mji wakaja wakitetemeka kumlaki na kusema, “Je, umekuja kwa amani?” 5Akasema, “Ndio, kwa amani; nimekuja kutoa dhabihu kwa Bwana. Jitakaseni na mje pamoja nami kwenye dhabihu.” Kisha akawatakasa Yese na wanawe na kuwakaribisha kwenye dhabihu. 6Walipofika, akamwona Eliabu na kufikiri, “Hakika masihi wa Bwana yuko hapa mbele Yake.” 7Lakini Bwana akamwambia Samweli, “Usiangalie uso wake au urefu wa kimo chake, kwa maana nimemkataa; kwa kuwa Bwana haoni kama mwanadamu aonavyo, maana mwanadamu huangalia umbo la nje, bali Bwana huangalia moyo.” 8Kisha Yese akamwita Abinadabu na kumfanya apite mbele ya Samweli. Lakini akasema, “Bwana hajamchagua huyu pia.” 9Kisha Yese akamfanya Shama apite. Lakini akasema, “Bwana hajamchagua huyu pia.” 10Basi Yese akawafanya wanawe saba wapite mbele ya Samweli. Lakini Samweli akamwambia Yese, “Bwana hajawachagua hawa.” 11Kisha Samweli akamwambia Yese, “Je, hawa ndio vijana wote?” Naye akasema, “Bado yupo mdogo, lakini tazama, anachunga kondoo.” Basi Samweli akamwambia Yese, “Tuma mtu kumleta, kwa maana hatutaketi chini mpaka atakapokuja hapa.” 12Basi akatuma mtu kumleta. Sasa alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri na sura ya kupendeza. Bwana akasema, “Inuka, mpake mafuta; kwa maana huyu ndiye.” 13Kisha Samweli akachukua pembe ya mafuta na kumpaka mbele ya ndugu zake; na tangu siku hiyo na kuendelea, Roho wa Bwana alikuwa na nguvu juu ya Daudi. Samweli akaondoka na kwenda Rama.
Fungua katika kisoma Biblia ↗