Luka 24:13-35 (OTB)
13Siku hiyo hiyo, wawili kati yao walikuwa wakielekea kijiji kimoja kiitwacho Emau, kilicho umbali wa karibu stadi themanini kutoka Yerusalemu. 14Walikuwa wakizungumza wao kwa wao juu ya mambo yote yaliyotokea. 15Walipokuwa wakijadiliana mambo haya, Yesu mwenyewe akakaribia na kuanza kutembea pamoja nao; 16lakini macho yao yalizuiliwa wasimtambue. 17Akawauliza, “Ni mambo gani haya mnayozungumza mnapotembea?” Wakakaa kimya, wakiwa na huzuni. 18Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa, akajibu, “Je, wewe ndiye mgeni pekee huko Yerusalemu asiyejua mambo yaliyotokea huko siku hizi?” 19“Ni mambo gani?” Akauliza. Wakajibu, “Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa nabii mwenye nguvu katika matendo na maneno mbele za Mungu na watu wote, 20na jinsi wakuu wa makuhani na watawala wetu walivyomsaliti ili ahukumiwe kifo, na kumsulubisha. 21Lakini tulitumaini kwamba ndiye atakayemkomboa Israeli. Na zaidi ya hayo yote, hii ni siku ya tatu tangu mambo haya yalipotokea. 22Zaidi ya hayo, baadhi ya wanawake wetu walitushangaza. Walikwenda kaburini alfajiri na mapema 23na hawakuona mwili wake. Walikuja wakisema wameona maono ya malaika, waliowaambia kwamba yu hai. 24Kisha baadhi ya wale waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini na wakakuta kama vile wanawake walivyosema, lakini hawakumwona.” 25Akawaambia, “Enyi wapumbavu, na wenye mioyo mizito kuamini yote waliyosema manabii! 26Je, haikupaswa Kristo kuteseka mambo haya na kisha kuingia katika utukufu wake?” 27Na akianza na Musa na manabii wote, akawafafanulia yaliyoandikwa katika Maandiko yote kumhusu yeye mwenyewe. 28Walipokaribia kijiji walikokuwa wakienda, alifanya kana kwamba anaendelea mbele zaidi. 29Lakini wakamsihi sana, wakisema, “Kaa nasi, kwa kuwa ni karibu jioni; siku imekwisha.” Basi akaingia kukaa nao. 30Alipokuwa akikaa nao mezani, akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuanza kuwagawia. 31Ndipo macho yao yakafunguliwa na wakamtambua, naye akatoweka machoni pao. 32Wakaulizana, “Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu alipokuwa akizungumza nasi njiani na kutufunulia Maandiko?” 33Wakaondoka saa hiyo hiyo na kurudi Yerusalemu. Huko wakawakuta wale kumi na mmoja na wale waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika pamoja 34wakisema, “Bwana amefufuka kweli kweli na amemtokea Simoni.” 35Ndipo wale wawili wakasimulia yaliyotokea njiani, na jinsi alivyotambuliwa nao katika kumega mkate.
Fungua katika kisoma Biblia ↗